National News

DC KIGOMA AZINDUA ZAHANATI YA KAMALA BANGWE TAYARI KWA KUTOA HUDUMA

Tarehe: 11 Nov, 2023


Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ndugu. Salum Kali amezindua Zahanati mpya ya Kamala- Bangwe iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa lengo la kuanza kutoa huduma za afya kwa Wananchi. 

Akihutubia Wananchi katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya amewataka Wakazi wa eneo hilo kutunza miundombinu ya Zahanati na kuwataka Wahudumu wa afya kutumia lugha nzuri katika kuhudumia Wagonjwa.

Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhe. Baraka Naibuha Lupoli  amesema Manispaa hiyo imelenga katika kusogeza huduma karibu na Wananchi kwa kutekeleza miradi ya Maendeleo ambapo kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa Ofisi za Kata za Kisasa kwa kila Kata huku akisema mpango wa Ujenzi wa Zahanati ni kwa kila Kata.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Bi.Mwantum Mgonja amesema Ujenzi wa Zahanati hiyo umegharimu kiasi cha fedha za Kitanzania zaidi ya Million Mia moja na sita (Tsh 106, 292, 060/=) na vifaa tiba vikigharimu kiasi cha Million hamsini (Tsh 50, 000, 000/=) fedha kutoka Serikali Kuu. 

Amesema kwa kipindi cha uongozi wa Rais Dr. Samia Suluhu Hassani Manispaa hiyo imepokea Fedha za Kitanzania zaidi ya Tsh Billion 3.4/= katika utekelezaji wa miradi ya afya na ununuzi wa vifaa tiba.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Dr. Hashim Mvogogo amesema Zahanati hiyo inaanza kutoa huduma kwa Wagonjwa wa Nje (OPD), Maabara na huduma za Mama, Baba, na Mtoto (kliniki) ambapo pia vyumba vya mapumziko vipo katika jengo hilo. 

cc:kigomaujijimc

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab